HABARI


............................................................................

Vikongwe wauawa kwa ‘kuroga’ mvua
WANAWAKE watatu wazee wa kijiji cha Usevya, wilayani Mpanda wameuawa na wananchi wakituhumiwa kuroga mvua isinyeshe. 

Imedaiwa kuwa mvua haijanyesha kijijini hapo tangu msimu wa mwaka huu wa kilimo uanze na kusababisha ukame. 

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Rukwa, Isuto Mantage, aliwataja waliouawa kuwa ni Consolata Nsokilo (64) na Oliveta Pesambili (74) na mwingine wa tatu ambaye jina lake halikuweza kupatikana mara moja, lakini anakadiriwa kuwa na umri wa kati ya miaka 75 na 80. 

Kwa mujibu wa Kamanda Mantage, tukio hilo lilitokea juzi saa 3.30 usiku katika kijiji hicho. Imedaiwa kuwa siku iliyofuata, baada ya mauaji hayo mvua kubwa ilinyesha kwa zaidi ya saa moja kuanzia saa nne asubuhi na kuibua hisia tofauti miongoni mwa wakazi wa Usevya. 

Kwa mujibu wa mashuhuda ambao hawakutaka kutajwa majina gazetini, usiku wa tukio kundi la wanakijiji wenye silaha za jadi; mapanga, marungu, mawe na fimbo, walivamia nyumba za wabibi hao na kuwashambulia na kuwaua kikatili. 

Ilidaiwa kuwa kabla ya kuwaua, wananchi hao waliwalazimisha kufanya kila wawezalo ili mvua inyeshe lakini waliwaeleza kuwa hawakuwa na uwezo huo huku wakilia na kubembeleza wasiwaue kwa kuwa wao si wachawi na wala hawajihusishi na mambo ya kishirikina. 

Kwa mujibu wa Kamanda Mantage, ‘wauaji’ hao walitawanyika mara moja kutoka eneo la tukio baada ya kutekeleza unyama huo na polisi wanaendesha msako wa kuwatia mbaroni ili sheria iweze kuchukua mkondo wake. 

Mauaji hayo yametokea siku chache baada ya mauaji ya imani za kishirikina kutokea Songea, Ruvuma na kusababisha machafuko yaliyosababisha vifo vya watu watatu, wawili wakiwa wameuawa na polisi katika maandamano na mmoja kwa ajali ya pikipiki. 

Kila mara Serikali pamoja na vyombo vya Dola, wamekuwa wakitoa miito ya kuyakataza mauaji ya imani za kishirikina ambayo yalipata kukithiri mkoani Shinyanga dhidi ya vikongwe. 

Lakini pia yamekuwapo mauaji ya wenye ulemavu wa ngozi kwa imani kwamba viungo vyao vinaweza kusababisha utajiri. 

Watu kadhaa walishakamatwa kuhusiana na mauaji hayo na kuchukuliwa hatua za kisheria.