MICHEZO / SPORTS NEWS

...................................................................

Mosha ajiuzulu umakamu Yanga
MAKAMU mwenyekiti wa  klabu ya Yanga, Davis Mosha amejiuzulu uongozi  huo kwa kile alichokieleza kuwa amechoshwa na masimango ikiwa ni pamoja na matusi ambayo amekuwa akitukanwa na mashabiki mara kwa mara.Akizungumza na Mwananchi jana, Mosha alisema kuwa baadhi ya wanachama wa klabu hiyo wamekuwa wakimpa wakati mgumu kiasi cha kuhatarisha maisha yake.

"Nimemkabidhi barua rasmi kwa mwenyekiti jana (Lloyd Nchunga), nahisi kama ninapoteza fedha zangu nyingi, gari langu wamenivunjia vioo,najitolea kwa kila hali kuisaidia klabu, lakini huko sithaminiwi wala watu hawaoni umuhimu wangu, napoteza muda wangu bure hakuna faida yoyote bora niachane nao niangalie mambo yangu mengine," alisema Mosha

"Hebu fikiria sasa hivi wananituhumu kuwa nimehujumu mechi yetu  na  Simba, nihujumu kwa sababu gani, nimechoka bwana kutukanwa ovyo kama mtoto, nimewaachia klabu yao, majungu yanatawala hapo kuna watu wapo pale hawataki kufuata katiba, ukiwaambia fuateni na kuiheshimu katiba ndiyo iliyotuingiza madarakani unaundiwa zengwe sasa hayo maisha gani, nimechoka mimi,"alisisitiza.

Tangu aingie madarakani mwaka jana, Mosha   amekuwa akitofautiana na aliyekuwa mdhamini wao, Yusuf Manji ikiwa ni pamoja na mwenyekiti wake, Nchunga katika maamuzi mbalimbali yanayohusu klabu hiyo ya Mtaa wa Twiga na Jangwani.Alipoulizwa kuhusu kujiuzulu kwa Mosha, Kaimu Katibu Mkuu wa Yanga, Selestin Mwesingwa alisema, "Ni kweli amejiuzulu amenipa nakala ya barua yake hapa, lakini suala hilo mwenyekiti atalitolea ufafanuzi siku yoyote kuanzia sasa.

Hivi ninavyokwambia nipo kwenye mchakato wa kuwajulisha wajumbe wengine wa kamati ya utendaji kuhusu uamuzi huo wa Mosha."Ni jambo la kusikitisha kuona kiongozi anajiuzulu kwa sababu ya wanachama, wanambughudhi mtu mpaka anaamua kuchukua maamuzi mazito kama hayo, kamati ya utendaji itakaa sasa sijajua kama itabariki kujiuzulu kwake au la,"alisema Mwesingwa.

Naye  Nchunga hakuweza kupatikana jana kuzungumzia suala hilo kutokana na simu yake ya kiganjani kuita kwa muda mrefu bila majibu.



Hashem Thabit auzwa

 mtanzania wa kwanza kucheza katika ligi ya NBA,Hasheem Thabeet aliyekuwa akichezea timu ya Memphis Grizzlies, ameuzwa kwenda timu ya Houston Rockets ya jijini Houston,Texas katika mabadilishano maalumu baina ya timu hizo mbili.
Katika mabadilishano hayo,mchezaji Shane Battier aliyekuwa akichezea timu anayokwenda Hasheem(Houston Rockets) anajiunga na Memphis Grizzlies.

Maendeleo ya Hasheem katika ligi hiyo ya NBA yamekuwa hayaridhishi. Ana kiwango cha vikapu 1.2 na rebound 1.7 kwa kila mchezo. Hicho ni kiwango cha chini sana kwa mchezaji ambaye alichaguliwa akiwa kama 2nd pick katika draft mwaka 2009.Aliyekuwa 1st pick katika mwaka huo ni Blake Griffin aliyekwenda Los Angeles Clippers.
Ni matumaini yetu kwamba kwa kwenda Houston mji ambao unaaminika kuwa na watanzania wengi zaidi nchini Marekani kuliko mahali pengine, Hasheem atajisikia kuwa “nyumbani” zaidi na atapata muda wa kucheza zaidi kitu ambacho anakihitaji sana ili kuendeleza mchezo wake ndani ya ligi hiyo yenye ushindani wa kila aina. Kila la kheri Hasheem.
.................................................................................